UMUHIMU WA CHANJO KWA WATOTO

Posted on: September 4th, 2023

Leo tarehe 4 Septemba 2023 wataalamu wa afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga wamepatiwa semina elekezi kuhusiana na umuhimu wa kukamilisha chanjo kwa watoto.

Akizungumza na watumishi hao Afisa Ufuatiliaji wa magonjwa yanayotibika kwa chanjo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) anayeshughulikia mikoa ya Nyanda za juu kusini mwa Tanzania Dkt Boniface Makelemo amesema kupitia semina hiyo wanawakumbusha wataalamu wa afya kuhusiana na umuhimu wa chanjo na  kuangalia na kutambua hali ya chanjo kwa  watoto wanaoletwa Hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Amesema kupitiwa utaratibu huo wa kuhakiki na kutambua hali ya chanjo kwa watoto endapo watabainika hawajakamilisha chanjo kuwekwe utaratibu wa kuwapeleka katika vituo vya karibu vinavyotoa huduma ya chanjo ili kukamilisha chanjo hizo.

Ameongeza kuwa kuna umuhimu kukazania na kukamilisha chanjo kwa watoto kwani imesaidia kuboresha afya za watoto kwa kuepuka  magonjwa yanayozuilika na chanjo na kufuta ugonjwa kama Ndui na kupunguza ugonjwa wa Polio, Surua na magonjwa ya kuhara.