UZINDUZI WA CHANJO YA POLIO
Posted on: September 21st, 2023
Leo tarehe 21 Septemba 2023 Kampeni maalum ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio imezinduliwa rasmi mkoani Rukwa.
Akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Charles Makongoro Nyerere amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuruhusu watoto walio chini ya umri wa miaka minane kupata chanjo ya matone dhidi ya Ugonjwa wa Polio kwa siku nne kuanzia leo tarehe 21 mpaka tarehe 24.
Kutokana na uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Polio na ukaribu uliopo wa mipaka ya kijografia na muingiliano wa kijamii na kiuchumi kati ya mikoa sita na nchi jirani ametoa wito kwa wakuu wa mikoa na wilaya kupitia kamati za afya za msingi za mikoa na halmashauri ambayo kampeni hii ya chanjo itafanyika Rukwa, Kagera, Kigoma, Mbeya, Katavi na Songwe kusimamia kampeni hii maalum ya chanjo dhidi ya Ugonjwa wa polio kwa watoto walio chini ya umri wa miaka minane.
Aidha ametoa wito kwa taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali, wadau mbalimbali wawe sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya chanjo ya polio.
Tarehe 26 Mei 2023 Wizara ya afya kupitia mfumo wa upimaji na ufatiliaji kwa wahisiwa wa Ugonjwa wa polio ilipokea taarifa ya uwepo wa mtoto mmoja wa umri wa mwaka mmoja na miezi kumi mwenye dalili ya ugonjwa wa Polio kata ya Malangali Manispaa ya Sumbawanga Mkoa wa Rukwa na vipimo vya maabara vilithibitisha uwepo wa ugonjwa huo.
Ili kuzuia ugonjwa huu usiendelee amesema serikali kupitia wizara ya afya inaendelea kuchukua hatua stahiki kukabiliana na ugonjwa huo kwa kuchanja watoto walio chini ya umri wa miaka minane na kuimarisha huduma za chanjo, kutoa elimu kwa jamii namna ya kujilinda na ugonjwa huo ikiwemo usafi, kuepuka chakula na kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi, kufanya tafiti kuhusu magonjwa yanayozuilika kwa chanjo na kuongeza ushirikiano kwa jamii pamoja na kushirikiana na wadau kudhibiti ugonjwa wa Polio.